MIAKA 40 YA NEEMA KWA WAAGUSTINO TANZANIA.
|
Nyumba ya waagustino Mahanje- Songea |
Wakati Shirika la Mt. Augustino Tanzania
linatimiza miaka arobaini (40) tangu lilipoanza kufanya utume wake hapa
Tanzania katika Parokia ya Mt. Mikael Mahanje Jimbo kuu la Songea tarehe 9 mwezi
Desemba 1977. Baada ya kupita mwaka
mmoja mapadre Augustino Perez na Vitalino Malagon wakijifunza lugha na
utamaduni wa kitanzania, wakakabidhiwa Parokia na walikuwa wameingia Tanzania
22.5.1976. Katika miaka hiyo 40 ya utume shirika limepanuka kufanya utume wake
sehemu mbalimbali za Tanzania. Baada ya kufanya utume wake takribani miaka kumi
na tisa (19) katika Parokia ya Mt. Mikael Mahanje Songea, 28.8.1996 ilizinduliwa nyumba ya Malezi Morogoro eneo la Kola Hill
kwa ajili ya wanafunzi wa falsafa na teologia na kuanza kutoa huduma ya
kichungaji katika vigango viwili kwa parokia mbili tofauti. Kigango cha Pangawe
Jeshini ambacho kipo chini ya Parokia ya Mgolole na kigango cha Bwawani ambacho
kipo chini ya Parokia ya Chalinze.
Jinsi watawa walivyozidi ongezeka ndivyo na utume
ulianza kupanuka 6.1.2001
ikazinduliwa Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili Mavurunza ambacho
kilikuwa kigango cha Parokia ya Msewe-Ubungo Jimbo Kuu Katoliki la Dar es
Salaam. Mwezi Januari 2007 ikazinduliwa
Parokia ya Mt. Augustino Mkolani katika Jimbo kuu la Mwanza. Haikupita muda
mrefu Agosti 2009 ikazinduliwa Parokia nyingine ya Mt. Augustino Temboni Dar es
Salaam. Baadaye Januari 2013 Parokia ya Mt. Ambrose Tagaste Dar es Salaam. Pia 1.5.2016 Parokia ya Mt. Rita wa Kashia
na mwaka huo huo 21.12.2016 Parokia
ya Mt. Monika Buhongwa Jimbo Kuu la Mwanza.
|
Parokia ya Waagustino Enduimet Arusha |
Licha ya huduma za Parokiani kumekuwa pia na shughuli
nyingine za malezi zilizopelekea kupata mapadre wazalendo wenye kuhudumia
parokia hizi. Zaidi ya hayo kuna sekondari.
SHUGHULI
ZA MALEZI
Mwaka 1978 walianzisha shughuli za malezi kwa wanaotaka kuwa
watawa katika shirika. Malezi haya yalikuwa yanafanyika Mahanje, baadaye
kupanua uwigo ikafunguliwa nyumba ya malezi Morogoro kama tulivyoona huko juu.
Nyumba hiyo ilizinduliwa 28.8. 1996
kwa ajili ya wanafunzi wa falsafa na teologia. Na wakawa wanaenda kufanya
noviciate Intramuros Manila Ufilipino. Hivyo imefanyika hivyo kwa miaka kadhaa.
Lakini wengi wao hawakuweza kuendelea baada ya kurudi toka novitiati na wengi
waliacha siku chache kabla ya kwenda.
Mwaka 2011 ikiwa ni maazimio ya mkutano Mkuu wa kati wa
Shirika Duniani uliofanyika Ufilipino Septemba 2010 wenye kusistiza unovisi wa
pamoja. Basi mwaka 2011 kundi la kwanza lilianza malezi ya novitiate 1.7.2011 katika Parokia ya Mt.
Augustino Mkolani kwa kuunganisha delegation ya Tanzania na Kenya. Malezi hayo
yamekuwa yakiendelea miaka yote hadi sasa.
|
Parokia ya Mt. Alipio Mkolani Mwanza |
Pamoja na malezi ya kitawa pia mwaka 2014 shule ya sekondari ya Mt. Augustino Tagaste Dar es Salaam na
kuanza kupokea wanafunzi mwaka huo. Mwaka huu 2017 wanamaliza kwa mara ya
kwanza vijana wa kidato cha nne. Hadi sasa vijana wamekuwa wakifanya vizuri
katika mitihani ya taifa ya kidato cha pili na pamoja na kikanda au kimkoa. Tunamatumaini
makubwa kuwa kundi hili la kidato cha nne na hata wanaofuata watafanya vizuri
katika mitihani yao ya kitaifa.Malezi yao si tu elimu dunia bali pia elimu
Mungu na maadili mema.
Mwaka
2017 mwaka wa Neema
Shirika la Mt. Augustino Tanzania mwaka huu umekuwa ni wa
neema na mwaka wa kumshukuru Mungu kwa sababu zifuatazo:
Tarehe 8.7.2017
waliweka nadhiri za kwanza vijana wanne katika nyumba ya novitiate iliyopo
katika Parokia ya Mt. Augustino Mkolani, Mwanza. Kati ya hao wane mtanzania ni
mmoja. Pia kwa mwaka huu kwa mara ya kwanza kabisa tangu shirika liingine
Tanzania kupata daraja la upadre vijana sita kwa mara moja. Hayo ni mafanikio
ya kuanza malezi kwa ngazi zote hapa Tanzania. Walipewa daraja la upadre 27.7.2017 Madaba Songea. Pia vijana
wanne (4) waliweka nadhiri za daima katika nyumba ya malezi Morogoro 10.8.2017.
|
Sekondary ya Mt. Agustino Tagaste Dsm. |
Pamoja na
matukio ya nadhiri na upadrisho Delegation ya Tanzania imepata parokia tatu
ndani ya mwaka mmoja nazo ni: 20.7.2017
ilizinduliwa parokia ya Enduimet umasaini katika Jimbo kuu la Arusha, 27.7.2017 Parokia ya Mt. Augustino
Madaba, Jimbo Kuu la Songea na 20.8.2017
Parokia ya Mt. Josephine Bakhita Korona, Jimbo Kuu la Arusha.
Tunawashukuru maaskofu waliotupokea katika majimbo yao.
Kwa hiyo hadi sasa utume wetu hapa Tanzania tunafanya katika majimbo yafuatayo:
Jimbo Kuu la Songea katika Parokia
ya Mt. Mikael Mahanje na Mt. Augustino Madaba. Jimbo Kuu la Dar es Salaam: Katika Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa
dhambi ya asili Mavurunza, Mt. Augustino Temboni, Mt. Ambrose Tagaste, Mt. Rita
wa Kashia….. pia Sekondari ya Mt. Augustino Tagaste. Katika Jimbo Kuu la Mwanza: Parokia ya Mt.
Augustino Mkolani, na Mt. Monika Buhongwa. Jimbo
la Morogoro: Nyumba ya malezi Mlima Kola Morogoro. Jimbo Kuu la Arusha: Parokia ya Enduimeit na Mt. Josephine Bakhita
Korona.
|
Parokia Mt, Agustino Temboni Dsm |
Hadi sasa delegation ya Tanzania imekuwa na idadi
ya mapadre watanzania wapatao 31 na
mabradha 3 pia mafrateri
wanaojiandaa kwa daraja la ushemasi halafu upadre 4. Na kufanya idadi ya wana nadhiri za daima kuwa 38 idadi inayokaribia kwa idadi ya
province ambayo ni 40. Pamoja na
idadi hiyo wapo waprofesi wa muda wapatao 11,
wanovisi 3 na wapostulanti 9. Hivyo tunasababu za kutosha
kumshukuru Mungu kwa zawadi ya miito katika Delegation yetu na kuomba Mungu
tuweze kufanikiwa katika ombi la kuwa vicariate kwani kikatiba idadi
imejitosheleza na kupita kabisa. Idadi inayotakiwa ya chini ni watawa 20 na
miradi yenye kuwezesha watawa kujitegemea.
|
Nyumba ya Mt. Agustino Morogoro |
|
Nyumba ya Mt. Alipio Mkolani Mwanza |
Pindi ambapo Tanzania inafanya jubilei ya miaka 100 ya
Upadre, Waagustino tunaungana na wote katika kumshukuru Mungu kwa mchango wetu
wa miaka 40 ya utume hapa Tanzania. Tunamshukuru Mungu kwa miaka 40 sasa tangu
waagustino kwa mara ya kwanza tukabidhiwe Parokia ya Mahanje tumeendelea
kulitangaza neno la Mungu kwa roho ya kiagustino yaani: Kuishi kwa pamoja kama
ndugu tukiwa na Moyo Mmoja na Roho Moja njiani kwa Mungu. Kwani umetufanya Ee bwana na Mioyo yetu haitulii
mpaka ifike kwako (Conf.1.1).
Hatunabudi kama Delegesheni kumtolea Mungu shukrani kwa neema alizo tujalia kwa
kipindi chote hiki na kuzidi kumwomba aendelee kumimina neema zake kwa miaka
ijayo ya kulieneza neno la Mungu lililo kiini cha furaha kamili ya Mwanadamu.
Pd. Efrem Msigala, OSA
Mkolani Mwanza 2017
Nivema kumshukuru Mungu kwa neema zake. Sifa na utukufu viwe kwa Mungu Daima. Endeleeni kutenda kazi mkihudumia taifa la Mungu bila Kuchoka.
ReplyDelete